Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt.Adam Fimbo
NA. JIMMY KIANGO
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewatangazia waingizaji bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi kuwa mifumo ya TANCIS-TRA na RIMS-TMDA imeunganishwa ili kuongeza ufanisi katika kuingiza na kutoa shehena za bidhaa hizo nchini kwa njia ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt.Adam Fimbo, Aprili 8,2026, lengo kuu la kuunganisha mifumo hiyo ni kurahisisha michakato ya uombaji vibali kuwa na sehemu moja ya kuingiza taarifa, pamoja na kuboresha ufuatiliaji na shughuli za udhibiti wa maombi ya kuingiza na kutoa bidhaa nchini.
“Hivyo mnajulishwa rasmi kuwa kuanzia Mei 1, 2026 maombi yote yaliyokuwa yanapitia TMDA-RIMS na TRA-Forodha kwa ajili ya kutoa taarifa (declaration) yatafanyika moja kwa moja katika mfumo wa TANCIS.
“Ili kuepusha hoja zisizo za lazima na kurahisisha huduma za upatikanaji wa vibali, mnakumbushwa kuzingatia usahihi wa taarifa za bidhaa zinazosimamiwa na TMDA (ikijumuisha namba za usajili za bidhaa na majengo); na wadau wote watatakiwa kushirikiana na Wakala wa Forodha kwa ukaribu ili kuthibitisha usahihi wa taarifa za kitaalam na nyaraka hitajika.”
Taarifa hiyo imeweka wazi kuwa tangazo hilo linawahusu waingizaji wa mizigo mikubwa ya forodha, na si waingizaji kwa matumizi binafsi (personal use).
0 Comments