Ticker

7/recent/ticker-posts

LATRA: UPANGAJI WA NAULI HAZINGATII BEI YA MAFUTA PEKEE

 


NA. FATMA JALALA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeeleza kuwa upangaji wa nauli za usafiri wa umma hauamuliwi na bei ya mafuta pekee, bali huzingatia mchanganyiko wa vigezo mbalimbali vinavyoathiri gharama za uendeshaji.


Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habibu Suluo, amesema vigezo hivyo ni pamoja na bei ya vyombo vya usafiri, gharama za vipuri, mishahara ya wafanyakazi na rejesho la uwekezaji kwa watoa huduma.


Amesema mchanganyiko huo husaidia kupata nauli halisi inayoendana na hali ya soko na kuhakikisha uendelevu wa sekta ya usafiri wa umma.


“Bei ya mafuta ni sehemu tu ya vigezo vinavyochochea mapitio ya nauli, si kigezo pekee cha kuamua kupanda au kushuka kwake,” amesisitiza.


Dkt. Suluo ameongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni za tozo za mwaka 2020, mtoa huduma anaweza kuwasilisha mapendekezo ya mapitio ya nauli au mamlaka yenyewe kuanzisha mchakato huo inapobidi.


Akizungumza katika mkutano wa wadau uliofanyika Aprili 8, 2026 katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, amesema lengo ni kuhakikisha nauli zinaakisi gharama halisi za uendeshaji.


Naye, Andrew Magombana wakati akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, aliwataka wadau kuwasilisha maoni yao, hususan namna mabadiliko ya bei ya mafuta yanavyoathiri shughuli zao.

Post a Comment

0 Comments