Ticker

7/recent/ticker-posts

WATUNZA KUMBUKUMBU KUJENGEWA UWEZO WA KITAALUMA


 NA MWANDISHI WETU-AFRINEWSSWAHILI-DSM

Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kinatarajia kutoa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo watunza kumbukumbu wa Serikali na Binafsi.

 

Mafunzo hayo yamepangwa kufanyika Mei 6-9, 2024 mkoani Iringa kwenye ukumbi wa Masiti Grand Hall, na yatahusisha wataalamu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. 

 

Mwenyekiti wa chama hicho Devotha G. Mrope ndie aliyetoa taarifa hiyo juzi Aprili 8,2024 katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 

 Amesema mafunzo haya yanalenga kuwawezesha watumishi wa umma na taasisi binafsi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na uadilifu katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.

 

"Mafunzo haya yatawakilisha juhudi za TRAMPA katika kujenga uwezo na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini Tanzania. 

 


"Tunajitahidi kuhakikisha wataalamu wetu wanapata mafunzo na maarifa yanayohitajika ili kutunza vema taarifa na nyaraka kwa weledi na uadilifu,"  amesema  Devota.

 

Ameongeza kuwa hiyo ni fursa kwa washiriki kujifunza mbinu mpya na  bora za utunzaji wa kumbukumbu, uadilifu katika utunzaji wa siri za ofisi, na njia za kisasa za usimamizi wa nyaraka za taasisi.

 

Pia, kwa kuzingatia thamani ya mafunzo hayo, washiriki watalazimika kulipia gharama ya ushiriki ambayo ni shilingi laki nne tu (400,000), ambayo itagharamia uendeshaji wa mafunzo kwa muda wa siku nne. 

 

Sambamba na hilo, Devotha ametoa wito kwa waajiri kuwawezesha watumishi wao kuhudhuria mafunzo hayo na kuwalipa stahiki zao. 

 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wanataaluma

kuthibitisha ushiriki wao mapema ili kurahisisha maandalizi ya mafunzo hayo muhimu.

 

“Kada hii ni miongoni mwa kada zinazoongozwa na mifumo mingi, sambamba na miongozo kulingana na wakati. Hivyo, inalazimu wataalamu wajengewe uwezo kuendana na mazingira ya wakati husika,” amesisitiza Devotha.



Post a Comment

0 Comments