Mchakato wa kutunga kanuni za Habari unaelekea kukamilika hivyo Serikali imeshauriwa kukutana na wadau wa Habari nchini ili kuzipitia kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, wakati wa kikao cha siku moja cha Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), kilichoitishwa na Jukwaa hilo.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt.Anna Henga, ameshauri kanuni za habari ambazo zipo njiani kutungwa, zipoze suala la makosa ya kihabari kuitwa uchochezi.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kililenga kupitia vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari vilivyopitishwa na Bunge mwaka huu, pia kuangalia mwelekeo wa Kanuni za Habari ambazo zipo njiani kutungwa.
“Sera ya habari inayokuja, ipooze hili suala la wanahabari kuitwa wachochezi. Iondoe yale makosa ya jinai, suala la kupashana habari halipaswi kuwa na jinai ndani yake,” alisema.
Dkt.Henga alisema, suala la kupashana habari ni haki ya kikatiba, makosa yanaweza kutoka kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote hivyo, kufanya makosa hayo ya kitaaluma kuwa jinai, ni kuifinya tasnia ya habari.
“Katiba yetu Ibara ya 18 inasema, mtu ana haki ya kutoa, kupokea na kupata habari. Kanuni zetu zizibe ile mianya inayomtia mashaka mwanahabari,” alisema Dkt.Henga.
Pia, alishauri serikali kuendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wanahabari kama ilivyo nia ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba, inawezekana sheria kurejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho hata kama haijaanza kutumika.
“Wito wangu, sheria haikatazi kufanya mabadiliko ya sheria mara kwa mara, kwa kuwa sheria ya habari bado ina kasoro, inaweza kupelekwa tena bungeni na kurekebishwa,” alisema.
Kwa upande wake Mhdhiri kutoka SJMC, Dkt. Darius Mukiza, alishauri mafunzo kuhusu sheria ya habari yanapaswa kutolewa vyuoni.
“Mambo yote kuhusu sheria ya habari yanapaswa kuingizwa kwenye vyuo vya habari, vijana wanatoka vyuoni wakiwa hawajui chochote kuhusu sheria hizi,” alisema Dkt.Mukiza.
Nae Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF, Neville Meena, amesema wanahabari wasio na sifa ya elimu inayohitajika katika tasnia ya habari, wanapaswa kushinikizwa kufanya hivyo kwa kuwa fursa ipo.
“Tutakuwa watu wa ajabu kama tutaendelea kukumbatia watu wasio na sifa kwenye tasnia ya habari, fursa ipo tuwahimize ili wawe na sifa,” alisema Meena.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN, James Marenga, alisema, hatua ya Bodi ya Ithibati kusimamiwa na serikali inanyima uhuru wanahabari kujisimamia.
“Bodi ya Ithibati wajumbe wake wanateuliwa na waziri, inasimamiwa na waziri kwa maana ya serikali na ndicho chenye mamlaka ya kusimamia waandishi na hata kuwanyang’anya leseni. Hili linanyima uhuru wanahabari,” alisema Marenga.
0 Comments