Na MWANDISHI WETU - Afrinews Swahili- Dsm
Kuwepo kwa viumbe vamizi kwenye uhifadhi kumekuwa miongoni mwa sababu inayochagia kuathiri mazingira na kufifisha kasi ya ongezeko la vivutio vya utalii nchini.
Mtaalamu kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Joseph Olila, ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam, wakati wa kujadili changamoto za viumbe vamizi kwenye uhifadhi na maendeleo ya jamii ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Olila amesema viumbe vamizi vinahusisha aina ya mimea, wanyama au kiumbe chochote kile kinapoingia sehemu kwa mara ya kwanza na kuleta uharibifu.
“Kimazingira kiumbe vamizi kina tabia ya kuleta kuondoa viumbe vya asili na chenyewe kutawala eneo husika jambo linalosababisha kuleta madhara ya uharibifu wa uotoa wa asili, hatua hii inaathiri viumbe vilivyopo.”
Aidha amesema pia kuna changamoto kadhaa za kimazingira ambazo husababisha magonjwa. "Viumbe asili vinakuwa havina kinga wala kuandaliwa kibiolojia kumudu changamoto hiyo, ujio wa viumbe vamizi vinawaathiri.”
Akizungumzia changamoto za kijamii amesema kuwa viumbe vamizi vinatabia ya kuvuruga mimea, kusababisha magonjwa na kwamba changamoto hizi zote zinategemeana.
“Mfano kuna changamoto za kiuchumi. Hii tunaona kwamba gharama za kuwadhibiti viumbe hawa ni kubwa sana kwani zinahusisha vifaa na watu, hivyo vinapoingia kwenye mfumo wako wa uzalishaji gharama za kudhibiti zinakuwa kubwa.
“Pia inaathiri sana utalii, kwani inapotokea kwa muda mrefu kuwa viumbe vamizi wanyama wanapungua jambo ambalo linapunguza watalii kwani mazingira asili yanakuwa yametoweka.
“Hii ni sambamba na kwenye kilimo ambapo wanapoingia wanakuwa wanachochea gharama za kuondoa viumbe hivi,” amesema Olila.
Akizungumza namna ya kudhibiti viumbe hivyo, John Noronha ambaye ni Meneja Ufuatiliaji kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili amesema, kwanza ni kuhakikisha kuwa viumbe hivyo haviwezi kuingia kwenye mfumo wa uzalishaji
“Sababu ya kuzuia ushamiri wa viumbe hivi ni pamoja na kutokuwapo kwa viumbe ambavyo vinamtegemea kwa chakula. Pia kutoa uelewa mpana kwa jamii na wadau wengine juu ya viumbe hivi.
“Matharani
kuna viumbe kama Siam Weed huyu ndiye kiumbe anayesumbua kwa kiwango kikubwa
katika sekta ya wanyama nchini Tanzania, hivyo ni wajibu wetu kuendelea kutoa
elimu,” amesema Noronha huku akitaja baadhi ya wanayama wanaosababisha mgongano
kama Tembo, Simba, Fisi na wengine.
“Sambamba na hayo pia bado kuna changamoto ya upungufu wa sheria, mfano: kama wewe umelima kwenye kingo ya hifadhi basi hautafidiwa, vitu kama hivi vinapaswa kuangaliwa,” amesema.
Upande wake, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda maalum ya Dar es Salaam, Msafiri Kasara amesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan walioko katika Wilaya zenye mapori hatua ambayo imesaidia kuimarisha ulinzi.
“TAWA tumeweka utaratibu kwamba asilimia 25 ya pato ambalo linapatikana katika pori linalozunguka wananchi linakuwa ni la kwao.
“Hii hatua hii inasaidia mwananchi kutofanya ujangili, hadi kufikia sasa Sh. bilioni 37 zimetumika kwa ajili ya malipo hayo, mbali na hilo tumeweka kipaumbele cha huduma muhimu kama shule na zahanati,” amesema.
Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru, akifungua mjadala huo alisema mafunzo ya bayonuai ni muhimu katika uhifadhi wa mazingira nchini.
“Tunafundisha jamii na kuelimisha pia kuhusu sera, lengo likiwa ni kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi katika uhifadhi wa bayonuai kupitia vyombo vya habari,” amesema Dkt. Otaru.
JET imekuwa na utaratibu wa kukutana makundi mbalimbali yakiwamo ya wanahabari kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu nyanja tofautitofauti zinazohusu mazingira nchini.
0 Comments