Mmoja wa wanahisa wa kampuni ya Microsoft na Mtendaji Mkuu wa Masuala ya Teknolojia ndani ya kampuni hiyo maarufu duniani, Dkt. Nathan Myhrvold, leo Juni 25, 2023, amekamilisha mapumziko yake ya kiutalii katika Hifadhi ta Taifa za Nyerere na Ruaha.
Mfanyabiashara huyo ambae pia amehudumu kwenye kampuni hiyo kwa miaka 14 kwenye nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Tekolojia, ameondoka nchini na familia yake wakiwa na furaha.
Kabla ya kuja Tanzania, Dkt. Nathan alishawahi kuzungumza na Watendaji wa Wizara ya Utalii ulioongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, Mei 9, 2023 walipokutana nchini Marekani, ambapo aliahidi kuja Tanzania kupumzika.
“Ninavutiwa sana na vivutio vya utalii vya Tanzania. Nimeshafika Serengeti na Ngorongoro huko nyuma na safari hii nimebahatika kutembelea Ruaha na Nyerere haya ni miongoni mwa maeneo mazuri sana duniani. Tumefurahia sana,” alisema Nathan ambae amekuja nchini kwa ndege yake binafsi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas alisema ni faraja kwa tajiri huyo kutimiza ahadi yake.
“Ni faraja kwamba tulipokuwa kule Seattle, Marekani na kupata fursa ya kukutana naye pamoja na mipango mingine aliyokuwa nayo alishawishika kuja Tanzania tena na tumemsikia hapa mwenyewe akisema amefurahia akiwa na familia yake na leo kwa niaba ya Mhe Waziri wetu Mhe. Mohamed Mchengerwa, tumefika hapa kuwapa zawadi kidogo na kuwaaga,” alisema Dkt. Abbasi, akiwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Bw. Damasi Mfugale.
Dkt. Nathan, pamoja na kuwa na hisa kwenye kampuni za Microsoft na taasisi ya Intellectual Venture ambayo ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu, pia amewekeza pamoja na Bill Gates katika kampuni nyingine kubwa ya utafiti wa masuala ya Umeme salama ya TerraPower. Anatajwa kuwa mmoja wa wanasayansi na wagunduzi wakubwa wa nyakati hizi na mmoja wa wagunduzi wa programu ya “microsoft windows,” akiwa pia ni mwandishi mwenza na Bill Gates wa kitabu mashuhuri duniani kiitwacho “The Road Ahead.”
Kupitia taasisi yake ya Intellectual Ventures, Nathan anatajwa kuwa miongoni mwa Wamarekani watatu wanaomiliki kisheria ugunduzi wa masuala mbalimbali ya kisayansi na kuzitumia kibiashara hakimiliki zenye thamani ya mabilioni ya fedha.
Dkt. Nathan ambaye kwa upande mwingine pia ni mtafiti wa sayansi za vyakula na amejenga maabara maalum ya utafiti wa vyakula akiandika pia mfululizo wa vitabu viitwavyo “Modernist Cuisines: The Art and Science of Cooking,” ameeleza kufurahishwa na ladha za baadhi ya vyakula alivyokula Tanzania kama ugali, mtori na supu ya mbuzi. Ameahidi kuendelea na tafiti za vyakula vya Tanzania.
0 Comments