Ticker

7/recent/ticker-posts

WAWEKEZAJI KUTOKA UGANDA WAJITOSA KUWEKEZA KWENYE UMEME TANZANIA

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba (nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Col Mwesigye Fred (wa tatu kulia), Katibu Mkuu Wizaya ya Nishati, Athumani Mbuttuka( wa tatu kushoto), Kamishna Msaidizi Maendeleo ya umeme, Mhandisi Styden Rwebangila(kushoto) na wawekezaji kutoka Uganda kuhusu kuwekeza katika mradi wa umeme, Machi 21, 2023.


Na Zuena Msuya, Dodoma

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uganda nchini Tanzania pamoja na wawekezaji kutoka nchini humo kuhusu kuwekeza katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Lindi, Masasi, Tunduru na Songea.

Mazungumzo hayo yamefanyika Machi 21, 2023 katika ofisi za Wizara ya Nishati mkoani Dodoma na kuwashirikisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, Kamishna Msaidizi Maendeleo ya umeme, Mhandisi Styden Rwebangila na wawekezaji kutoka Uganda.

Wawekezaji hao wamemueleza Makamba kuwa wanataka kuwekeza katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo mkubwa wa Kilovolti 400 wenye urefu wa Kilometa 222.3 kutoka Lindi, Masasi hadi Songea.


Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba(kushoto) akizungumza na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Col Mwesigye Fred (wa pili kushoto) na wawekezaji kutoka Uganda kuhusu kuwekeza katika mradi wa umeme, Machi 21, 2023. Wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizaya ya Nishati, Athumani Mbuttuka.

Wawekezaji hao watawekeza kwa kusanifu, kutafuta fedha, kujenga na kuendesha njia hiyo na kuikabidhi baada ya muda uliopangwa.

Hata hivyo Makamba ameridhia wawekezaji hao kuwekeza katika mradi huo na kusema kuwa huo ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele kwa taifa.

Vilevile amewaagiza wawekezaji hao kukutana na Shirika la Umeme nchini Tanzania na maafisa wa Wizara ya Nishati ili kujadiliana na kuona njia bora ya kutekeleza mradi huo kwa kuangalia sheria, taratibu na kanuni za uwekezaji katika miradi ya umeme.

Aidha Wawekezaji hao pia wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika mradi wa umeme wa jua katika Kisiwa cha Mafia wenye megawati 5 kwa gharama ya Dola za Kimarekani  milioni 11.64.

Hata hivyo Waziri Makamba aliwaeleza wawekazaji hao kuwa serikali imeshapata kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 5 kutoka Wakala wa Maendeleo wa Ufaransa (AFD) na kwamba iko katika mazungumzo ya AFD ili  kuongeza fedha Zaidi.


Waziri January Makamba(kulia) akiwa na mazungumzo na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Col Mwesigye Fred (kushoto) na wawekezaji kutoka Uganda.

Balozi Col. Mwesigye Fred ameishukuru Serikali ya Tanzania, kwa kukubali wawekezaji kutoka nchini Uganda kuwekeza katika miradi ya umeme.

Amesema hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili ulioasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo.

Post a Comment

0 Comments