Ushirikiano wa NCMC na IETA kufungua milango ya uwekezaji wa kijani, kuongeza utaalamu na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya mikopo ya kaboni duniani.
Tanzania
imeongeza kasi ya kujiimarisha katika soko la kimataifa la kaboni baada ya
Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Centre
– NCMC) kusaini Mkataba wa Maelewano (MoU) na Chama cha Kimataifa cha Biashara
ya Uzalishaji wa Gesi Chafuzi (International Emissions Trading Association –
IETA), hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, utaalamu wa kiufundi na
ushiriki wa wadau katika maendeleo ya soko la kaboni nchini.
Mkataba huo
umesainiwa jijini Antalya, Uturuki, na Mtendaji Mkuu wa NCMC, Bi. Ngenda
Kathryn Kigaraba, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa IETA, Bw. Andrea Bonzanni.
Hafla hiyo
imeshuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo,
Dkt. Richard Muyungi.
Ushirikiano huo
unakuja wakati ambapo biashara ya kaboni inazidi kuwa nyenzo muhimu katika
juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku nchi
mbalimbali zikijitahidi kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kutafuta vyanzo
vipya vya fedha kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo
endelevu.
Kupitia
makubaliano hayo, Tanzania inatarajia kunufaika na uzoefu wa kimataifa katika
kujenga uwezo wa kitaalamu, kuboresha sera, kuimarisha mifumo ya usimamizi na
kubadilishana maarifa yatakayosaidia kuendeleza soko la kaboni lenye uwazi,
ufanisi na uadilifu wa kimazingira.
SOKO LA KABONI NI NINI?
Kwa uelewa mpana, soko la kaboni ni mfumo wa kiuchumi unaowezesha biashara ya mikopo ya kaboni (Carbon Credits) inayotokana na shughuli zinazopunguza, kuzuia au kuondoa hewa ukaa na gesi nyingine chafuzi zinazochangia ongezeko la joto duniani.
Kwa kawaida,
mkopo mmoja wa kaboni unawakilisha tani moja ya hewa ukaa (CO₂) au kiwango kinacholingana na tani moja ya gesi nyingine
chafuzi kwa kuzingatia uwezo wake wa kuchangia ongezeko la joto duniani.
Mikopo hiyo
inaweza kuzalishwa kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo uhifadhi na urejeshaji wa
misitu, upandaji miti, matumizi ya nishati safi, uzalishaji wa nishati
jadidifu, usimamizi bora wa taka, kilimo endelevu na teknolojia zinazopunguza
uzalishaji wa gesi chafuzi.
Katika mfumo
huu, taasisi au kampuni zinazotekeleza miradi inayozalisha upunguzaji wa hewa
ukaa uliothibitishwa zinaweza kupata mikopo ya kaboni na kuiuza kwa wanunuzi
wanaotaka kukidhi mahitaji yao ya kisheria au malengo yao ya hiari ya
kukabiliana na uzalishaji wa gesi chafuzi.
Hata hivyo,
mikopo hiyo haiwezi kuuzwa kwa kutegemea madai pekee ya kupunguza uchafuzi.
Inahitaji kufanyiwa tathmini, ufuatiliaji, uthibitishaji na uhakiki kwa
kuzingatia viwango vinavyotambulika ili kuhakikisha upunguzaji wa hewa ukaa
unaodaiwa umetokea kweli.
Kwa Tanzania,
mfumo huu unaweza kufungua fursa za uwekezaji katika misitu, kilimo, nishati,
usimamizi wa taka na sekta nyingine, huku ukiwawezesha wawekezaji na jamii
zinazotekeleza miradi hiyo kupata manufaa ya kiuchumi sambamba na kulinda
mazingira.
MKATABA
WA PARIS KUFUNGUA FURSA ZA KIMATAIFA
Moja ya maeneo
muhimu yaliyoainishwa katika mkataba huo ni utekelezaji wa Kifungu cha 6 cha
Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Kifungu hicho
kinaweka msingi wa ushirikiano wa nchi katika biashara ya matokeo ya upunguzaji
wa uzalishaji wa gesi chafuzi, ikiwa ni pamoja na kuhamisha mikopo ya kaboni
kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa kufuata taratibu zilizokubaliwa kimataifa.
Kwa mujibu wa
Mkataba wa Paris, Kifungu cha 6.2 kinawezesha nchi kushirikiana na kuhamisha
matokeo ya upunguzaji wa hewa ukaa kati yao, yanayojulikana kama Internationally Transferred Mitigation
Outcomes (ITMOs).
Kwa upande
mwingine, Kifungu cha 6.4 kinaanzisha mfumo wa kimataifa wa utoaji mikopo ya
kaboni chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama Paris Agreement Crediting Mechanism (PACM).
Mifumo hii ina
umuhimu mkubwa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania kwa sababu inaweza kuvutia
uwekezaji wa kimataifa katika miradi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi,
kuhamasisha teknolojia mpya na kuongeza upatikanaji wa fedha za kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo,
biashara hiyo inahitaji kuzingatia kanuni za uhasibu wa kaboni ili kuepusha
hali ya upunguzaji mmoja wa hewa ukaa kuhesabiwa mara mbili na nchi tofauti.
Kwa miamala inayohitaji marekebisho ya uhasibu wa kitaifa, nchi husika
zinapaswa kutumia utaratibu wa Corresponding
Adjustments kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 6.
TANZANIA
KUJIPANGA KATIKA SOKO LA KABONI LA ANGA ZA KIMATAIFA
Eneo jingine
muhimu katika ushirikiano huo ni Mpango wa Kimataifa wa Kupunguza na Kufidia
Uzalishaji wa Kaboni katika Usafiri wa Anga (Carbon Offsetting and Reduction
Scheme for International Aviation – CORSIA), unaosimamiwa na Shirika la
Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Mpango huo
unalenga kushughulikia ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa katika safari za
kimataifa za ndege kwa kutumia mikopo ya kaboni inayokidhi vigezo maalumu vya
ICAO, sambamba na hatua nyingine za kupunguza uzalishaji.
Kwa Tanzania,
uelewa wa mfumo huu unaweza kusaidia kuandaa miradi ya kaboni yenye viwango
vinavyoweza kukidhi mahitaji ya masoko maalumu ya kimataifa, ikiwemo yale
yanayohusiana na sekta ya usafiri wa anga.
Ni muhimu
kuelewa kuwa si kila mkopo wa kaboni unaozalishwa nchini unakubalika moja kwa
moja katika CORSIA. Mikopo hiyo lazima itokane na programu na mifumo inayokidhi
vigezo na kuidhinishwa na ICAO.
MSINGI
WA KISHERIA NA FURSA ZA UWEKEZAJI TANZANIA
Hatua hii ya
ushirikiano inajengwa juu ya jitihada ambazo Tanzania imeanza kuzitekeleza
katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni.
Mwaka 2022,
Serikali ilianzisha Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Biashara ya Kaboni
(Environmental Management (Control and Management of Carbon Trading)
Regulations, 2022), kupitia Tangazo la Serikali Na. 636 la mwaka huo.
Kanuni hizo
zilifanyiwa marekebisho mwaka 2023 kupitia Tangazo la Serikali Na. 721, hatua
iliyosaidia kuboresha mfumo wa kisheria unaosimamia biashara ya kaboni.
Aidha, Tanzania
ina Mwongozo wa Kitaifa wa Biashara ya Kaboni unaoweka taratibu na mahitaji ya
utekelezaji wa miradi ya biashara ya kaboni nchini.
Mifumo hiyo
inaweka msingi wa usajili na usimamizi wa miradi, tathmini ya athari za
kimazingira na kijamii, uthibitishaji wa upunguzaji wa uzalishaji, pamoja na
ushiriki wa wadau katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa hiyo,
ushirikiano wa NCMC na IETA unatarajiwa kuongeza uwezo wa kutumia mifumo hiyo
kwa kuzingatia mabadiliko ya taratibu za kimataifa na mahitaji ya wawekezaji.
UADILIFU
WA SOKO NA MANUFAA KWA JAMII NI MUHIMU
Pamoja na fursa
zinazotokana na biashara ya kaboni, wataalamu wa mazingira wanaeleza umuhimu wa
kuhakikisha soko hilo linaendeshwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na manufaa
yanayogusa jamii zinazoshiriki katika miradi.
Hii inahusisha
kuhakikisha kuwa miradi ya kaboni inatoa upunguzaji halisi wa gesi chafuzi,
inalinda mifumo ya ikolojia, inaheshimu haki za jamii na kuweka wazi namna
mapato yatakavyogawanywa kati ya waendelezaji wa miradi na wananchi
wanaochangia utekelezaji wake.
Vilevile,
uthibitishaji huru, ufuatiliaji wa muda mrefu na kuepusha kuhesabu upunguzaji
wa hewa ukaa mara mbili ni mambo muhimu katika kujenga imani ya wanunuzi na
wawekezaji.
Kwa mantiki
hiyo, ushirikiano kati ya NCMC na IETA una umuhimu wa kuongeza uelewa wa
masuala hayo na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, taasisi za Serikali na
wadau wengine katika maendeleo ya soko la kaboni nchini.
Kwa upande wa
kimataifa, IETA ni taasisi inayoshirikisha sekta mbalimbali katika kukuza
mifumo ya biashara ya uzalishaji wa gesi chafuzi, ikijikita katika uwazi wa
masoko, viwango vya uhasibu wa kaboni na utekelezaji wa mifumo ya biashara ya
kaboni chini ya Mkataba wa Paris.
SAFARI
YA TANZANIA KUELEKEA UCHUMI WA KIJANI
Kwa ujumla,
mkataba huo unatoa fursa ya kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uchumi wa
kijani unaozidi kupata umuhimu katika biashara na uwekezaji wa kimataifa.
Kupitia
ushirikiano huo, Tanzania inalenga kuongeza ushiriki wake katika mipango ya
kimataifa ya biashara ya kaboni, kuimarisha imani ya wawekezaji, kukuza
utaalamu wa ndani na kuongeza uwezekano wa kupata fedha za kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Fedha hizo
zinaweza kusaidia utekelezaji wa Mchango wa Kitaifa wa Tanzania katika
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Nationally Determined Contribution –
NDC), ambao unaainisha malengo na hatua za nchi katika kupunguza uzalishaji wa
gesi chafuzi na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo,
mafanikio ya ushirikiano huo hayatapimwa kwa kusainiwa kwa mkataba pekee, bali
kwa uwezo wa kuugeuza kuwa matokeo yanayoonekana kupitia uwekezaji, miradi yenye
ubora, ulinzi wa mazingira na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.
Hivyo, hatua
inayofuata ni kuhakikisha kuwa utaalamu na maarifa yatakayopatikana kupitia
ushirikiano huo yanawafikia pia wataalamu wa ndani, sekta binafsi na jamii
zinazotekeleza miradi ya kaboni, ili Tanzania iweze kutumia rasilimali zake za
asili kama sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi endelevu.

0 Comments