Ticker

7/recent/ticker-posts

MRADI WA KILIMO ENDELEVU WAWAONDOA WAKULIMA KWENYE MIKOPO YA KAUSHA DAMU ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mradi wa Kilimo Endelevu unaotekelezwa kwenye vijiji vya Seuri na Oldonyowas mkoani hapa, umeepusha wakulima na

mikopo ‘kausha damu’.


Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Island of Peace (IDP) na lingine lisilo la Serikali linalojihusisha na utafiti, ushauri wa

kitaalamu na Miradi ya Maendeleo na Jamii (RECODA) ukinufaisha zaidi ya wakulima 700 wa vijiji 10.


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wakulima wa vijiji hivyo walisema walishakata tamaa na

kilimo, kutokana na mavuno madogo waliyokuwa wakipata, ila tangu mradi huo uanze, wanaona matumaini mapya.

Mkulima Witness Sikoi wa Seuri, amesema IDP na RECODA wamemfanya aone kilimo kinalipa, kutokana na hatua aliyopiga.


Witness, Mwenyekiti wa Kikundi cha Elishorie, amesema kabla ya mradi wa Kilimo Endelevu wanawake wengi walishiriki mikopo inayotesa na kuwagombanisha na waume zao.


"Hatukuwa na amani kutokana na mikopo ya kausha damu, ila kwa sasa tuna amani isiyo na kifani, kwani tunalima eneo dogo

tunapata mavuno mazuri na soko la uhakika," amesema.


Amesema kwa sasa wameanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, hivyo wanaendesha maisha yao kwa upendo na amani.


Neema Augustino wa kikundi cha Faida, amesema mradi huo umewawezesha kupata elimu ya kilimo ikolojia, chenye manufaa kwa ardhi, mkulima na mlaji.

"Mradi wa Kilimo Endelevu umeniwezesha kupanda ndizi, kufuga nguruwe na kujiunga na vikoba, jambo linalonihakikishia kesho

yangu" amesema.


Neema alisema jambo la kupongeza ni wao kupata ushirikiano kwa waume zao, jambo ambalo halikuwapo siku za nyuma.


Mwalimu wa wakulima hao, Richard Kivuyo alisema wanufaika wanampa ushirikiano, jambo linalomrahisishia kutoa elimu

kirahisi.


Mkulima wa mbogamboga, Flora Molel wa Oldonyowas amesema kilimo ikolojia ni rahisi na chenye faida nyingi za kiuchumi,

kijamii na kiafya.


Amesema analima bilinganya, sukuma wiki, spinachi, saro, mnavu na mboga zingine zinazozalishwa kwa njia za kiikolojia.


"Bidhaa zangu zina uhakika wa soko, lakini pia nauza kwa njia ya mtandao, hivyo nina kipato cha uhakika," amesema.


Flora amesema kilimo ikolojia kimemtambulisha kitaifa, kwani

mwaka jana aliibuka mshindi wa kwanza katika wilaya ya Arusha.


Mkurugenzi Mkuu wa RECODA, Josephine Ng'ang'a amesema mradi huo umekuwa na matokeo chanya, ambapo baadhi ya

vikundi vimezaa vingine.


Josephine amesema pia wamekuwa wakishirikiana na Serikali kutekeleza miradi yao hasa kwa kufuata misingi ya RIPAT

yenye kaulimbiu ya ‘Njaa na Umasikini Inawezekana Kuwa Historia’.



Post a Comment

0 Comments