Ukweli ni kwamba Tamasha la Bongo Fleva Honors lililofanyika Mei Mosi 2026, jijini Dar es Salaam, ilikuwa kubwa na lilimependeza, ukizingatia na ukubwa wa msanii mwenyewe ambaye heshima yake ni kubwa sana nchini, Joseph Haule maarufu kama Professor Jay.
Prof. Jay, anatazamwa kama alama ya mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva, ambao leo hii unatazamwa kama moja ya maeneo muhimu yanayozalisha ajira nyingi kwa vijana wenye elimu na wasio na elimu.
Aidha harakagi kadha wa kadha za kuanzisha matamasha ya makubwa ya muziki nayo yanatajwa kuwa sehemu ya kuusukuma mbele muziki huu, kwa bahati mbaya sasa yapo matamasha ambayo wachambuzi wa masuala ya siasa wanayatazama kwa jicho kali kidogo kutokana na mwenendo wake kubeba vimelea vya kisiasa zaidi.
Miongoni mwake ni tamasha la Bongo Fleva Honors, hili ni tamasha lililobuniwa kwa lengo la kuwapa heshima wanamuziki wa zamani wa muziki huo, ukweli ni kwamba jukwaa la tamasha hilo hupambwa kwa burudani za hali ya juu, mathalani kwenye tamasha la mwishoni mwa wiki iliyopita mashabiki walifurika, na kwa ujumla tasnia ya muziki wa kizazi kipya ilionekana kung’ara kwa kiwango cha kimataifa.
Hata hivyo, pamoja na uzuri wote huo, kwa upande mwingine kulikuwa na hisia na vimelea vya kisiasa, wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa tamasha hilo linapaswa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.
Wengi wanaamini kuwa kama halitafungamanishwa na siasa hasa zikihusishwa na mmiliki wa tamasha hilo, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, basi lingekuwa ni tamasha la kiwango cha juu zaidi, ambalo hata wasanii wa nje wangetamani kushiriki.
Mjadala mkubwa ulizuka kufuatia tukio la kuzuiwa kwa Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, kusema neno jukwaani. Kwa wachambuzi wa burudani na wadau wa sanaa, hili halikuonekana sawa, kwani tamasha la aina hii linapaswa kuwa jukwaa la umoja, si mgawanyiko.
Wengi walisisitiza kuwa Professor Jay ni msanii mkubwa anayependwa na watu wa rika na itikadi zote, hivyo ni vyema matukio ya heshima kwake yakabaki kwenye misingi ya burudani kuliko visasi au tofauti za kisiasa.
Zaidi ya yote, mjadala wa heshima ya Bongo Fleva uliibuka kwa nguvu. Ni wazi kuwa muziki huu umejengwa na waanzilishi wake kama Professor Jay na wengineo, lakini pia umeendelea kung’ara kupitia kizazi kipya cha wasanii wanaoupeleka kimataifa kama Diamond Platnumz na Ali Kiba. Hivyo basi, heshima ya Bongo Fleva ni ya wote kwa maana ya walioianzisha na wanaoikuza.
Wapo wanaoona kuwa endapo Sugu ataweka pembeni siasa, tamasha hili linaweza kuwa alama kubwa ya sanaa nchini siku za mbeleni. Kwa sasa, baadhi ya wadau wanahisi kuwa linaelekea kuchukua taswira ya kisiasa zaidi, jambo ambalo linaweza kupunguza mvuto wake kwa wapenzi wa burudani, hasa ukizingatia kuwa wapenzi wa burudani nchin pamoja na kuunganishwa na muziki, lakini kila mmoja ana itikadi zake za kisiasa.
Ndiyo maana haikushangaza kwa baadhi ya watu kuona hali iliyotafsiriwa kama “ki-familia,” ambapo baadhi ya viongozi waliingia ukumbini huku wengine wakizuiwa. Hali hii imeibua mjadala mpana kuhusu mipaka kati ya sanaa na siasa na ni wapi mstari unapaswa kuchorwa.
Kwa ujumla, Bongo Fleva Honors 2026 imeonesha uwezo mkubwa wa kuwa tamasha la kimataifa, lakini pia imeacha funzo muhimu, ili sanaa iendelee kung’ara, inahitaji kubaki huru, jumuishi, na yenye lengo la kuunganisha watu bila kujali tofauti zao za kisiasa ama kidini.
0 Comments