Ticker

7/recent/ticker-posts

NEMC YAPONGEZWA KWA KUBADILI MITAZAMO YA JAMII JUU YA MATUMIZI YA TAKA

 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Mhandisi Hamad Masauni.

*AGENDA YAWATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA

 NA. MWANDISHI WETU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Mhandisi Hamad Masauni, amelipongeza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa jitihada zake za kubadili fikra za jamii juu ya kuzigeuza taka kuwa fursa kwa kushirikiana na wadau wa mazingira.

 

NEMC kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Taasisi ya AGENDA For Environment and Responsible Development imekuwa ikifanya jitihada za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu taka na kuzigeuza kuwa fursa yenye manufaa ya kiuchumi na kimazingira.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka Duniani yaliyofanyika  Machi 30, 2026, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mhandishi Masauni amesisitiza umuhimu wa kuendeleza dhana ya Kupunguza, Kutumia tena na Kurejeleza taka (Reduce, Reuse, Recycle), sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “kupunguza taka katika sekta ya chakula.”

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi
"Taka siyo uchafu bali ni fursa; tukizisimamia vizuri tunaweza kuzigeuza kuwa rasilimali yenye thamani kwa maendeleo endelevu.” Amesema Waziri Masauni.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesisitiza kuendelea kwa utoaji wa elimu ya mazingira hususan shuleni kuanzia ngazi ya msingi, pamoja na kuimarisha mafunzo kwa makampuni ya ukusanyaji taka kwa kushirikiana na NEMC ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa jamii ili kuongeza uelewa juu ya usimamizi bora wa taka na kuchochea ushiriki wa wananchi katika kulinda mazingira.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua thamani ya taka na kuzitumia kama rasilimali kwa maendeleo endelevu, huku yakiwakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira.
Afisa Program wa AGENDA, Clara Benjamin (kushoto)
AGENDA YAHAMASISHA VIJANA

Kwa upande wake Afisa Program wa AGENDA, Clara Benjamin alitoa wito kwa vijana kushieiki katika kutunza mazingira na kuchangamkia fursa hiyo iliyopo kwenye taka.

 

“Moja ya Malengo ya AGENDA ni kuwahamasisha vijana kuchangamkia fursa hizi zinazojitokeza na kuachana na fikra za kugombania ajira, badala yake wanaweza kujiajiri wenyewe, wanapaswa kuchukulia suala la taka kama fursa kwao kwa kujiingizia kipato.

 

“Vipo viwanda ambavyo vijana wanaviendesha wenyewe kwa kuzalisha vyakula vya mifugo hasa kuku na hasa ukizingatia kuwa kwa jiji la Dar es Salaam biashara ya ufugaji wa kuku ni kubwa, hivyo ni wazi soko la chakula cha kuku lipo.”

Post a Comment

0 Comments