Ticker

7/recent/ticker-posts

IUCN, COCA-COLA,GWC,WRBWB KUTUMIA NJIA ZA ASILI KUTUNZA VYANZO VYA MAJI BONDE LA NGERENGERE NA RUVU

NA. JIMMY KIANGO-MOROGORO

IUCN Tanzania, kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu (WRBWB), wanatekeleza mradi wa kutumia njia za Asili za urejeshaji wa vyanzo vya maji na uongezaji wa maji katika Bonde la Ruvu, Tanzania (NbS4Water – Ruvu).

Mradi huo wa miaka mitatu utagharimu kiasi cha dola za Marekani 1,712,764 sawa na Shilingi ya Tanzania  bilioni 4.399 zilizotolewa na mshirika wa maendeleo nchini kampuni ya kuzalisha vinywaji baridi ya Coca-Cola kupitia taasisi ya Global Water Challenge (GWC).


Mradi wa NbS4Water – Ruvu umeanza kutekelezwa mwaka 2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028, ukilenga eneo la chanzo cha maji cha Ngerengere katika bonde dogo la Ruvu ndani ya Bonde la Wami-Ruvu.


Lengo kuu la mradi huo ni kuongeza ujazo wa maji kwa kutumia suluhisho za asili (NbS) katika kurejesha vyanzo vya maji na kusimamia rasilimali za maji kwa njia endelevu katika bonde la Ngerengere.

MALENGO YA MRADI

Kwa mujibu wa Mwakilishi Mkazi wa IUCN-Tanzania, Charles Oluchina, malengo ya mradi huo uliozinduliwa rasmi Machi 25,2026, mkoani Morogoro ni kuimarisha uwezo wa taasisi katika usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji katika ngazi ya vyanzo vya maji na bonde.

 

Malengo mengine ni kurejesha maeneo yaliyoharibika na kusimamia mifumo ya maji kwa njia endelevu kupitia matumizi ya asili na kukuza utunzaji wa maji kwa kuhamasisha shughuli mbadala za kiuchumi zilizo endelevu.


MAENEO MUHIMU YA MRADI

Oluchina alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine mradi umelenga pia kuimarisha uwezo wa taasisi katika usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, kurejesha na kusimamia mifumo muhimu ya vyanzo vya maji kwa kutumia njia za asili.


Eneo jengine ni kukuza kiwango cha utunzaji wa maji kupitia teknolojia na shughuli za maisha endelevu sambamba na  kufuatilia, kutathmini na kujifunza mbinu mpya za kuboresha mradi.



MATOKEO TARAJIWA

Matarajio ya watekeleza mradi huo ni kuona uwezo wa angalau vyama saba vya watuamiaji wa maji (WUAs) vinaimarika.


Ubora wa mgawanyo wa maji unaimarika, kurejelezwa kwa hekta 3,000 za maeneo yaliyoharibika, kuongezeka kwa maji kwa kiasi cha ML 584.77, wakulima 2,000 kuanza shughuli mbadala ikiwemo kilimo himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi, ufugaji nyuki, na ufugaji samaki. 


UZINDUZI WA MRADI 

Mradi ulizinduliwa rasmi na Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Bi. Rosemary Rwebugisa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri na lengo la uzinduzi huo lilikuwa ni kutambulisha rasmi mradi kwa wadau wa ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na jamii. 


Kupata uungwaji mkono wa kisiasa na dhamira ya utekelezaji wake, kujenga ushirikiano na kuoanisha vipaumbele vya wadau na  kuongeza uelewa na umaarufu wa mradi. 

UPANDAJI MITI

Uzinduzi wa mradi huo unaohusisha wilaya tatu za mkoani Morogoro ambazo ni Morogoro Manispaa -Ngerengere, Halmashauri ya Morogoro na Mvomero ulitanguliwa na upandaji miti katika eneo la Mindu, ambapo kulifanyika zoezi la kukabidhi miche ya miti kwa wakulima ikiwa ni ishara ya kuanza kwa urejelezaji wa mazingira.


CHANGAMOTO NA HATUA ZA UTEKELEZAJI

Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu, Mhandisi Elbariki Mmasi aliiambia AFRINEWSSWAHILI kuwa zipo changamoto kadhaa zinazolikabili bonde hili miongoni mwake zikiwa ni matumizi yasiyo endelevu ya maji, uvamizi wa vyanzo vya maji, ukataji miti, mmomonyoko wa udongo na uchafuzi wa maji. 


Hata hivyo katika kukabiliana na changamoto hizo zipo hatua kadhaa zimeainishwa katika kutekeleza mradi huo kwa ufanisi zikiwemo za kuimarisha vyama vya watumia maji, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti, kukuza shughuli mbadala za kipato na kufuatilia ubora wa maji.


Kuchukuliwa kwa hatua hizo kunatazamiwa kuleta matokeo chanya, ambayo ni kuimarishwa kwa vyama saba vya watumia maji (WUAs), kurejelezwa kwa hekta 3,000 za eneo lililoharibiwa, kuongezwa kwa ML 584.77 za maji na wakulima 2,000 kufaidika. 


Aidha mradi huo unatarajia kunufaisha watu 5,000 ambao kati yao asilimia 60 ni wanaume na asilimia 40 ni wanawake, Serikali za Mitaa, NGOs na sekta binafsi. 


Mradi huo utaongozwa na IUCN kw akipindi chote cha miaka mitatu kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu huku muwezeshaji mkuu ikiwa ni Coca-Cola kupitia Global Water Challenge

 

Post a Comment

0 Comments