NA VICTOR MAKINDA: MOROGOROChama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Morogroro mjini Mkoani Morogoro, kimefurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumteua Balozi Dkt Emanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, uamuzi ambao pia umeridhiwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kwa kuwa Dkt Nchimbi licha ya uweledi wake katika uga wa uongozi, anakijua vyema chama hicho.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Morogoro mjini, Fikiri Juma, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Morogoro kwa lengo la kuelezea namna chama hicho kinavyosimamia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020.
Fikiri alisema kuwa CCM imefanya chaguo sahihi kwa wakati sahihi kwa kumteua mtendaji mkuu wa chama aliyekulia ndani ya chama na anayekijua vyema chama hicho hivyo anao uwezo mkubwa wa kuendelea kukijenga na kukitetea chama kwa nguvu ya hoja hususani kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani 2025.
“Uteuzi wa Dkt Nchimbi kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama, umepokelewa vizuri na Watanzania wote, sisi wana CCM wa wilaya ya Morogoro mjini tunaungana na watanzania wenzetu kumpongeza kwanza Mwenyekitiwetu wa chama Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Kamati kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) kwa uteuzi huo makini ambao umelenga kuendelea kukipa nguvu chama chetu na kukifanya kiendelee kuaminiwa na watanzania “ Alisema Fikiri.
Fikiri aliongeza kusema kuwa historia ya uongozi wa Dkt Nchimbi ndani ya CCM na serikalini haiacho doa kwani amekuwa ni kiongozi mpenda haki na maendeleo huku akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi, hivyo anaamini kuwa uongozi wake ndani ya CCM, utakuwa na tija kubwa kwa chama hicho.
“ Sifa ya usikivu, ukomavu wa kisiasa, uanadiplomasia na uwepesi wake wa kuelewa na kujibu hoja kwa kutumia nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu ni sifa ambazo Dkt Nchimbi amejaaliwa nazo ambazo zinatutia matumaini makubwa wana CCM wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuwa chama chetu kitazidi kuwa imara.” Anasema Fikiri.
Fikiri anaongeza kuwa Dkt Nchimbi amepitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na amekuwa mwenyekiti wa umoja huo na nafasi nyingine nyingi ndani ya chama hicho kikongwe Afrika, hivyo anaamini kuwa amepikwa vya kutosha kuwa kiongozi mahiri kwa kuwa UVCCM ni tanuru la kupika viongozi mahiri.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM wilaya ya Morogoro, Fikiri anasema kuwa chama hicho kinajivunia kwa jinsi kilivyofanikiwa kutekeleza ilani ya chama kwa kiasi kikubwa wilayani Morogoro.
“ Ninampongeza Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood, baraza la Madiwani Manisapaa ya Morogoro na watendaji wa serikali wa nafasi mbali mbali kwa kufanya kazi kwa bidiii kuhakikisha wananchi wa Morogoro mjini wanaondokana na kero za maji, umeme, huduma za afya, elimu na ubora wa shughuli za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na biashara.” Anasema.
Anasema kuwa Manispaa ya Morogoro imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za jamii na maisha ya wakazi wake kwa kuwa CCM imejidhatiti kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020.
0 Comments