Ticker

7/recent/ticker-posts

MANENO YA KWANZA YA PAPA LEO XIV, ASISITIZA AMANI,AOMBA KUENDELEA NA BARAKA ZA HAYATI PAPA FRANCISCO KWA DUNIA


“Amani iwe nanyi nyote.”  Ndugu wapendwa kaka na dada. Hii ndiyo salamu ya kwanza ya Kristo Mfufuka, aliyeutoa uhai wake. Mchungaji Mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kundi la Mungu. 

 

Mimi ningependa pia salamu hii iingie mioyoni mwenu na ifike katika familia zenu, kwa watu wote, popote walipo. Kwa mataifa yote, kwa dunia yote. Amani iwe nanyi.

 

Hii ndiyo amani ya Kristo Mfufuka. Amani isiyo na silaha na inayovunja silaha, yenye unyenyekevu na uvumilivu. Inatoka kwa Mungu. Mungu ambaye anatupenda sisi sote bila masharti. Ingawa sasa, sisi hapa bado tunahifadhi masikioni mwetu sauti ile dhaifu lakini yenye ujasiri wa Papa Fransisko aliyeibariki Roma.

 

Papa aliyebariki Roma alitoa baraka yake kwa dunia, dunia nzima. Asubuhi ile ya Pasaka. Niruhusuni niendelee na baraka hiyo. Mungu anatupenda. Mungu anatupenda sisi sote. Na uovu hautashinda. Sisi sote tuko mikononi mwa Mungu.

 

Kwa hiyo, bila hofu, kwa kushikana mikono, tukiwa wamoja leo kwa mkono wa Mungu na kati yetu sisi kwa sisi, twende mbele. Tuwe wanafunzi wa Kristo. Kristo anatutangulia. Dunia inahitaji mwanga wake. 

 

Ubinadamu unamhitaji kama daraja la kufikiwa na Mungu na upendo wake. Tusidharau nafasi yetu katika kujenga madaraja ya mazungumzo, ya kukutana, ya kuungana sote ili kuwa taifa moja daima katika amani. Asante kwa Papa Fransisko.

 

Pia ningependa kuwashukuru ndugu makardinali wote walionichagua kuwa mrithi wa Petro na kutembea pamoja nanyi kama Kanisa lililo moja, likitafuta daima amani, haki, na kufanya kazi kama wanaume na wanawake wafuasi waaminifu kwa Yesu Kristo. Bila hofu, kwajili ya kutangaza Injili, kwaajili ya kuwa wamisionari.

 

Mimi ni mtoto wa Mtakatifu Agostino. Muagustino. Ambaye alisema “Pamoja nanyi ni Mkristo, kwa ajili yenu ni askofu.” Kwa maana hii sote tunaweza kutembea pamoja kuelekea nchi ile ya mbinguni ambayo Mungu ametutayarishia.

 

Kwa Kanisa la Roma, salamu maalum. Tunapaswa kuanza pamoja Kanisa la kimisionari. Kanisa linalojenga madaraja ya kufunguka na mazungumzo, daima lililo tayari kupokea. Kama uwanja huu, wenye mikono wazi kwa wote. Kwa wote wanaohitaji wema. Uwepo wetu, mazungumzo yetu na upendo wetu.

 

Na mkiniruhusu, pia neno la salamu kwa wote, na hasa kwa Jimbo langu pendwa la Chiclayo kule Peru, ambako waamini wamekuwa pamoja na askofu wao, wameishiriki imani yake na wamejitoa sana, ili kuendeleza Kanisa aminifu la Yesu Kristo.

 

Kwenu nyote, kaka na dada wa Roma, Italia, na duniani kote. Tunapenda kuwa Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalotembea, Kanisa linalotafuta daima amani, Kanisa linalotafuta daima huruma, Kanisa linalotafuta kuwa karibu nasi, zaidi sana kwa wale wanaoteseka.

 

AMEN

 

 

Post a Comment

0 Comments